Share news tips with us here at Hivisasa

Gavana wa Kaunti ya Nakuru Kinuthia Mbugua amewaonya wanaonyakuwa vipande vya ardhi vya umma akisema watajipata taabani hivi karibuni.

Akizungumza siku ya Jumatano alipokuwa akifungua rasmi kichinjio cha Kaunti ya Nakuru kwenye wadi wa Biashara, viungani mwa mji wa Nakuru, Gavana Mbugua alisema kuwa kipande kikubwa cha ardhi hiyo ya kichinjio tayari kimenyakuliwa.

“Ninawaonya watu ambao wana mtindo wa kunyakua mashamba au mali ya wananchi. Nawahakikishia kuwa nitafuatilia mali yoyote au shamba lolote la serikali ya Kaunti ya Nakuru ambalo limechukuliwa kinyume na sheria. Hata uwe umejenga au umeuzia mtu mwingine shamba hilo, mali yote ya umma lazima yatarudi kwa wananchi. Mtu mmoja hawezi kujitajirisha na mali ya umma,” alisema Mbugua.

Gavana huyo alisisitiza kuwa wajibu mkuu wa serikali yake ni kuwahudumia wakazi wake kwa kuhakikisha mazingira ambayo wakazi hao wanaishi ni ya kuridhisha na ambayo yanawazesha kujimudu maishani.

Aliongeza kuwa serikali ya Kaunti ya Nakuru imekabarati kichinjio hicho kilichojengwa mwaka wa 1943 na wafungwa wa vita vikuu vya pili kama mojawapo ya njia ya kutimiza lengo hilo.