Gavana wa Kaunti ya Kwale ambaye pia ni mwenyekiti wa Muungano wa Jumuiya ya Kaunti za Pwani Salim Mvurya amepuzilia mbali maadai kuwa muungano huo umefifia na haufanyi kazi.
Gavana huyo amesema kuwa kufikia sasa wamekuwa wakiweka mikakati na sheria za kuendesha shuguli za muungano huo ,na hivi karibuni watazindua sheria hizo baada ya makubaliano na maafisa wote katika kaunti husika.
Mvurya amesema haya siku moja tu baada ya mwenyekiti wa wabunge kutoka kanda ya Pwani ambaye pia ni Mbunge wa Kaloleni Mwinga Gunga kutoa madai kuwa Muungano wa Jumuiya ya Kaunti za Pwani haujafanya maendeleo yoyote kwa wakaazi wa Pwani.
Aidha, gavana Mvurya amewaonya viongozi dhidi ya kuingiza siasa kwa maswala ya jumuiya ya kaunti za Pwani, kwa kusema kuwa muungano huo unafaa kuleta maendeleo kwa wananchi na wala sio kuwanufaisha viongozi kisiasa.