Gavana wa kaunti ya Nyamira John Nyagarama amejitenga na shtuma kuwa kuna ufisaid na mapendeleo kwenye afisi yake kuhusiana na nafasi za ajira.
Haya yanajiri baada ya wakazi kulalamikia hali hiyo, na kumshtumu gavana kwa kunyamazia jambo hilo.
Akizungumza kwenye mahojiano katika kituo cha Radio ya Egesa siku ya Alhamisi, Nyagarama aliwashtumu wakosoaji wake akisema kuwa hausiki katika shughuli za uajiri wa wafanyakazi wa kaunti kwa maana kuna bodi ya uajiri wa wafanyakazi inayoshughulikia masuala ya uajiri.
"Wanaonishtumu kwa mapendeleo kwenye uajiri wa wafanyikazi na hata pia ufisadi serikalini wanakosea pakubwa kwa maana kuna bodi ya uajiri wa wafanyakazi inayoshughulikia masuala ya uajiri, na mimi siketi kwenye bodi hiyo ili kufanya maamuzi kuhusiana na wanaostahili kupewa ajira," alisema Nyagarama.
Akizungumzia suala la ufisadi linaloikabili serikali yake Nyagarama aliongeza kuwa serikali yake imekuwa ikishikiliana kwa ukaribu na tume ya kupambana na ufisadi nchini EACC huku akionya maafisa watakaopatikana wakijihusisha na ufisadi serikalini.
"Tumekuwa tukishirikiana kwa karibu na tume ya kukabili visa vya ufisadi humu nchini na hivi karibuni tume hiyo ilipotoa orodha ya kaunti fisadi, Nyamira ilijumulishwa miongoni mwa serikali za kaunti zinazorekodi visa vichache vya ufisadi, ila kamwe mimi binafsi siwezi vumilia visa vya ufisadi kwenye serikali yangu," aliongezea Nyagarama.