Kwa mara nyingine tena Gavana wa kaunti ya Nyamira John Nyagarama amejitokeza kuwaonya vikali mawaziri wazembe katika serikali yake.
Akiwahutubia wanahabari afisini mwake siku ya Jumanne, Nyagarama alisema kuwa kamwe hatowavumilia mawaziri wazembe wanaohudumu kwenye serikali yake huku akihoji kuwa sharti kila mmoja awajibike.
"Serikali yangu ina mipango ya kuhakikisha kuwa miradi mbalimbali tuliyoianzisha imekamilika kwa wakati ili kuwafaidi wananchi na hili halitafanikiwa ikiwa kazi ya baadhi ya mawaziri wangu ni kuketi afisini nakusoma gazeti," alionya Nyagarama.
Nyagarama aidha alichukua fursa hiyo kuwaomba wakazi wa kaunti ya Nyamira kuwa na subira kungoja serikali yake kumaliza miradi mbalimbali ya kimaendeleo kabla yao kuanza kuishtumu kwa kutetekeleza miradi muhimu.
"Baadhi ya watu wamekuwa wakilalama kwamba serikali yangu haijakuwa ikitekeleza miradi ya maendeleo, ila ningependa kuwaomba wawe na subira tunapoendelea kutekeleza miradi ya ukarabati wa barabara, ujenzi wa zahanati na hata kufungua vyuo vya kiufundi na kwa kweli hata mji wa Roma haukujengwa kwa siku moja," aliongezea Nyagarama.
Haya yanajiri baada ya baadhi ya wakazi wa kaunti hiyo kuishtumu serikali ya kaunti ya Nyamira kwenye vyombo vya kijamii kwa kutotekeleza miradi ya maendeleo.