Gavana wa Kaunti ya Kisii James Ongwae ameahidi kununua vifaa zaidi vya kupima magonjwa mbalimbali na kuajiri madaktari katika Hospitali ya Keera iliyoko wadi ya Nyatieko eneo bunge la Kitutu Chache kusini Kaunti ya kisii.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Akizungumza siku ya Jumanne katika hospitali hiyo ya Keera alipokuwa ameenda kutembelea miradi mbalimbali katika eneo hilo akiwa na mbunge wa eneo hilo Richard Momoima Onyonka, Ongwae alisema kuwa kuna upungufu wa madaktari pamoja na vifaa kama mashine za kupima magonjwa.

 Alisema kuwa kwa wiki tatu zijazo atakuwa ameshughulikia mambo hayo kikamilifu.

“Nimetembea katika hospitali hii na kuona vitu ambavyo vinahitajika. Hakuna mashine za kupima magonjwa mbalimbali na pia kuna ukosefu wa madaktari wa kutosha,” alisema Gavana Ongwae.

Aliongezea: “Wananchi husumbuka sana kuenda hadi hospitali ya kisii kutafuta huduma bora. Nitahakikisha kila kitu kimewekwa hapa ili muwe mnahudumiwa hapa.”

Wakati huo huo, Gavana Ongwae alitoa mabomba ya kupitisha maji katika hospitali hiyo huku akisema atashirikiana na mbunge wa eneo hilo kukwamua miradi ya maendeleo ambayo imekwama na kusema watahakikisha viwango vya elimu vimeinuka katika eneo hilo na sekta ya afya.

Kwa upande mwingine wakaazi wa eneo hilo walimshukuru Gavana Ongwae kwa kuwakumbuka haswa katika sekta ya afya ili wawe wanapata huduma bora ya matibabu.

“Tunasema asante kwa gavana kwa kusema atatuongezea madaktari na kununua vifaa vya hospitali hii. Tunamwomba aendelee kutukumbuka,”alisema Stevin Omariba, mkaazi wa eneo hilo.