Gavana wa Kaunti ya Kisii James Ongwae ameahidi kuwatambua na kuboresha maisha ya wanariadha kutoka Kisii walioiletea nchi ya Kenya sifa katika Nyanja za riadha miaka za awali kwa kuweka msuada bungeni na kuhakikisha mashujaa hao wanalipwa pesa kidogo ya kuwakimu kiuchumi.
Gavana Ongwae akiongea Jumatano katika Uga wa michezo wa Gusii Green katika hafla za kuadhimisha siku kuu ya Madaraka alisikitikia hali ambayo mashujaa hao wanaoishi baada ya kuiletea taifa la Kenya sifa nyingi kwenye riadha ambapo aliweza kuchukua nafasi hiyo na kumtambua mwanariadha mkongwe Nyantika Mayioro.
Ongwae alisema kuwa tayari kuna mswada katika Bunge la Kaunti ya Kisii ambao utashughulikia maslahi ya mashujaa wote kutoka Kaunti hiyo, kutoka vitengo mbali mbali hasa michezo aina yote kama riadha ambayo ilitoa Mwafrika wa kwanza kwa kushinda dhahabu mnamo mwaka 1953 kwenye Indian Ocean Games kule Madagascar kutoka Kaunti ya Kisii.
“Ninawaahidi wote waliopigania uhuru wetu pamoja na wale walioshiriki katika michezo ya kwanza ya riadha ambayo kwa bahati nzuri mshindi alitoka Kaunti hii yetu anayejulikana kama Nyantika Mayioro,” alisema Ongwae.
Naye Bwana Nyantika alimshukuru Gavana Ongwae kwa kumtambua kwa wakaazi wa Kisii huku akisema kuwa yupo tayari kushirikiana na Serikali ya Kaunti kwa kutoa ushauri kwa wanaridha wanaochipukia na kuwataka vijana wote kutoka Gusii kwa jumla kutilia maanani masuala ya michezo.