Gavana wa kaunti ya Kisii James Ongwae amewahakikishia wanabiashara wa soko ya Daraja Mbili kuwa soko hilo litaanza kukarabatiwa hivi karibuni.
Hii ni baada ya wanabiashara hao kulalamikia hali mbaya ya soko hiyo kwa mda mrefu, huku wengi wakilalamika kila mara na kutishia kuandamana kuhusu hali mbaya ya soko hiyo.
Akiongea katika mji wa Kisii, Ongwae alisema mikakati ambayo ilikuwa inawekwa kuhusu ujenzi wa soko hiyo imekamilika, huku sura ya ujenzi wa soko hiyo ikiwa mojawapo ya mikakati mbayo ilikuwa ikishughulikiwa.
“Serikali kuu imetukabidhi millioni 600 na sisi kama serikali tutaongeza pesa zingine ili ujenzi wa soko hiyo ukamilike na wanabiashara wawe wanafanya shughuli zao za ubadilishanaji kama kawaida,” alihoji Ongwae.
Ujenzi wa soko hiyo umekuwa ukisubiriwa kwa mda mrefu bila kuzaa matunda, lakini kwa sasa wakaazi wa kaunti hiyo wakiwemo wanabiashara wako na kila sababu ya kutabasamu baada ya gavana kukiri kuwa ujenzi utaanza katika soko hiyo kabla ya miezi miwili ijayo.
“Soko hii ya Daraja Mbili ni miongoni mwa soko kubwa zaidi magharibi mwa Kenya na hiyo ni ishara kuwa wanabiashara ni wengi hufanya ubadilishanaji wao katika soko yetu ya daraja,” aliongeza Ongwae.
Aidha, gavana Ongwae amesema kulingana na utafiti uliofanywa unaonyesha kuwa kaunti ya Kisii hukusanya ushuru nyingi zaidi katika mkoa wa Nyanza.
“Tunastahili kufunguliwa wakala ya benki hapa Kisii maana tunakusanya ushuru nyingi zaidi katika kaunti hii yetu lakini tutakuwa na maongezi na wahusika halisi,” alidokeza Ongwae.