Gavana wa Kaunti ya Kisii James Ongwae amewaomba viongozi wa Serikali za Kaunti nchini kushirikiana pamoja na kuinua viwango vya uchumi ya Kenya ili kufikia mahitaji ya wanainchi wote.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akiongea katika hafla ya mafunzo juu ya umuhimu wa kujiunga katika jumuia ya Africa katika mkahawa wa Ufanisi mjini Kisii siku ya Jumanne, Gavana Ongwae alitoa mfano jinsi nchi za Africa mashariki zimekuja pamoja na kutaka Kaunti zote nchini kuiga mfano huo kwa kuungana pamoja ili kuinua viwango vya maendeleo.

”Huu ndio wakati wa kuungana pamoja kwa Kaunti zetu ili tuinue uchumi wa nchi yetu na kusherekea matunda ya ugatuzi,” alisema Gavana Ongwae.

Hii imekuja wakati aliyewakilisha Kaunti ya Nyamira kutoka Bunge la Juimuiya ya Afrika Mashariki kusema barabara itakayojengwa ya kufikia mataifa ya Afrika Mashariki itapitia mji wa Kisii.

Akiongezea kuwa Kaunti zinazopakana na Kaunti ya Kisii zinastahili kuungana pamoja na kuleta soko la upamoja (common market) ili kujiinua na kuboresha biashara.

Aliziorodhesha Kaunti za Nyamira, Migori, Homa-Bay na Narok kama majirani wanaostahili kujiunga pamoja na kuinua viwango hivyo.

Aidha, Ongwae alisema kuwa wanastahili kujenga viwanda mbalimbali kusaidia mkulima wa kawaida ili wapate mahali pakuuza bidhaa zao.

Ongwae alidokeza kuwa Kaunti ya kisii wanaendelea na mazungumzo ya kujenga kiwanda cha miwa na punde tu mazungumzo hayo yatakapofikiwa kiwanda hicho kitajengwa.

Kwingineko alisema wakati Kaunti hizo zitaungana pamoja watapania jinsi ya kujenga viwanda mbalimbali katika Kaunti zao.

Ongwae alitumia Kaunti ya Kisii kama mfano kuanzisha kiwanda cha ndizi na aliongezea kuwa wataweza zungumza na Serikali ya Kaunti ya Nyamira ili kuanzisha kiwanda cha Parachichi.

Vile vile Ongwae aliomba watu kuunga mkono hatua ya jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuwa jumuiya hiyo  inatazamia kuleta maendeleo katika Afrika ya Mashariki.

Hafla hiyo iliandaliwa na wasimamizi wa East Africa Legislative Assembly (EALA) waliokuwa na funzo maalumu  kwa wenyeji wa Kisii na kuwaeleza umuhimu wa kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki.