Gavana wa Kaunti ya Kisii James Ongwae amewataka mawaziri wa kaunti hiyo kuwajibika katika kufanya kazi zinazohusiana na wizara zao na kuwahudumia wananchi vizuri. Gavana Ongwae akiongea jana katika kongamano aliloandaa kujadili uwekezaji kwenye kaunti hiyo, aliwataka mawaziri wote kuhakikisha kuwa wanahudumia wakaazi na kutekeleza majukumu yao bila upendeleo. "Tufanyie watu wetu kazi ipasavyo na tushirikiane vilivyo kuleta maendeleo katika kaunti yetu na kuboresha uchumi wetu," alisema Gavana Ongwae. Pia aliwaomba wawekezaji kuwa huru kwa kushirikiana na Kaunti ya Kisii ili kuwekeza katika kufungua nafasi za kazi kwa vijana ambao ndio uti wa mgongo wa ukuzaji wa uchumi wa nchi kwa jumla.

Share news tips with us here at Hivisasa

Hata hivyo mawaziri wa kaunti hiyo wamekuwa wakilaumiwa mara kwa mara na wakaazi kwa utendakazi usioridhisha kwa wafanyibiashara na wakazi. Haya yanajiri huku serikali ya kaunti ya Kisii ikiwa miongoni mwa kaunti zilizoorodheshwa miongoni mwa kumi bora katika uwekezaji na ukuzaji wa kiuchumi na shirika la utafiti la Infotrack.