Gavana wa Kaunti ya Kisii James Ongwae amewahakikishia wakaazi wa Kaunti hiyo kuwa atafanya maendeleo zaidi kabla ya mwaka huu kukamilika.
Akiongea siku ya Jumapili katika hafla ya kuchangisha pesa za ujenzi wa Kanisa ya St. Athony katoliki Marani ilioko katika Wadi ya Marani eneo Bunge la Kitutu Chache Kaskazini, Ongwae alisema mataa katika barabara yataongezwa zaidi katika eneo hilo la Marani, soko 30 zitakarabatiwa kikamilifu kwa Kaunti yake kabla ya mwaka huu kukamilika.
Aidha, Onwgae alitangaza kuwa Serikali yake imetenga fedha Sh240 milioni kwa sekta ya maji huku chemichemi 10 za maji zitakarabatiwa kwa kila Wadi za Kaunti hiyo.
Wakati huo huo, Ongwae alisema barabara zitakarabatiwa kikamilifu zikiwemo barabara ya Rioma–Esegesa-Kiomocha na kuunganisha barabara kuu ya Marani kuelekea Kegogi. Barabara nyingine aliahidi kuitengeza ni ya Nyagesenda–Masakwe hadi eneo la Sombogo.
Ongwae, aliongezea kuwa barabara ya kutoka eneo la Mbanda–Marani hadi Kegogi nayo itawekwa lami chini ya uongozi wa Mbunge wa eneo hilo la Kitutu Chache Kaskazini Jimmy Angwenyi.
Gavana Ongwae pia alisema Serikali yake imetenga pesa za ununuzi wa mbolea ili wakulima wakabidhiwe mbolea hiyo wakati huu wa upanzi.
Vile vile alisema sekta ya Afya atashughulikia kikamilifu hasa kwa Hospitali ya Kisii Levei Four huku akisema Hospitali ya Marani itapata mashine ya CT scan mwaka huu.
“Nina ushirikiano mwema na wawakilishi wote wa Wadi na tutahakikisha maendeleo yamefanyika kikamilifu na ipasavyo,” alisema Ongwae.
Viongozi wengine waliohudhuria hafla hiyo, ni Afisa wa Usalama katika Kaunti ya Kisii Patric Lumumba, Mwakilishi wa Wadi ya Marani Denis Ombachi na Mwakilishi wa Wadi ya Boigesa Edward Otuke huku Sh563,000 zikichangishwa.