Baaddhi ya wakaazi wa kaunti ya Kisii wamekasirishwa na hatua ya gavana wao, James Onwgae, ya kususia sherehe za leba dei.
Wakaazi wa kaunti hiyo walifika katika uwanja wa michezo wa Gusii wakimngoja gavana wao angalau awaelezee hatua alizozichukua kupunguza swala la ajira katika kaunti hiyo.
Jameson Araka mkaazi ni mmoja wa wale ambao walikuwa wamefika katika uwanja huo huku wakingojea hotuba ya gavana huyo.
“Mimi sina kazi tangu kaunti yetu kutuachisha kazi. Ingekuwa bora angefika katika mkutano huu atuelezee mipango kaunti yake iliyoweka kuangazia swala la kazi za kaunti,” alisema Araka.
Kwa upande wake Bob Omariba ambaye ni mwanabodaboda alighadhabishwa na hatua ya Ongwae akisema kuwa hakuonyesha uongozi bora.
"Nilidhani gavana atakuja. Ningefaidi upande wa abiria kwani watu waliposikia kuwa Ongwae hayuko wengi hawakuona haja ya kuhudhuria sherehe,” alisema Omariba.
Vilevile wachuzi nao hawakuachwa nje, Maria Motari alieleza masaibu yake ya kutembea kutoka Kegati hadi uga wa Gusii.
Biashara yake haikurekodi faida kama alivyo tarajia.
"Nilinunua 'stock' nyingi ya bidhaa hizi nyingine nimeweka hizi zikiisha nilete, sasa nimeenda hasara nilitumia nauli kutoka Kegati nikijua biashara ipo hapa lakini sioni matumaini," akasema Motari.