Gavana wa kaunti ya Nyamira, John Nyagarama, amejitenga na madai kuwa anatumia pesa za kaunti hiyo vibaya.
Akiongea siku ya Jumapili na waandishi wa habari katika mji wa Nyamira, gavana huyo alisema anazitumia pesa za kaunti hiyo vizuri katika miradi mbalimbali ambayo inainua kaunti hiyo kimaendeleo.
Hii ni baada ya seneta wa kaunti hiyo Kennedy Mong’are Okong’o kusema kuwa gavana wa kaunti hiyo alitumia pesa nyingi kupita kiasi kinachohitajika kwa ujenzi wa lango la hospitali ya kiwango cha tano, madai gavana amesema ni uwongo .
“Wananchi wa kaunti yangu wameridhika na wamefurahishwa jinsi maendeleo yanafanywa katika kaunti hii kupitia serikali yangu. Hayo mengine ya kusema kuwa natumia pesa vibaya si ya ukweli,” alisema Gavana Nyagarama.
Aidha seneta alikiri kuwa pesa nyingi zilitumika kwa ununuzi wa mashine za kupima magonjwa mbalimbali katika hospitali hiyo ya Nyamira na kumwagiza Gavana Nyagarama kutumia pesa za wananchi vizuri na kuweka kando matumizi mabaya ya pesa katika kaunti hiyo.
“Gavana wa kaunti hii anatumia pesa vibaya na hafanyi maendeleo inavyostahili. Namwomba atumie pesa za wananchi vizuri ili maendeleo yafanywe kikamilifu kwa wananchi wa kaunti hii,” alisema Seneta Okong’o.
Hii si mara ya kwanza seneta wa kaunti hiyo kumkosoa Gavana Nyagarama katika maendeleo. Seneta huyo hapo mbeleni alidai kuwa gavana hatengenezi barabara za kaunti hiyo hadi kiwango kile kinachohitajika.