Gavana wa Kaunti ya Nyamira John Nyagarama kupitia Wizara ya Kilimo alifadhili makundi mbali mbali idadi ya mbuzi 360 wa kufuga ili kuimarisha uchumi wa Kaunti hiyo.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akiongea siku ya Jumatano katika eneo la Nyamusi Wilayani Nyamira Kaskazini alipowakabidhi makundi hayo mbuzi 360, Nyagarama alikiri kuwa ndoto yake ni kuona Kaunti yake ikiinuka kiuchumi na kibiashara kupitia kilimo pamoja na ufugaji.

“Mbuzi hawa ni wa maziwa na nawaomba waliopata mbuzi hao kuwalinda vizuri na kuwalisha vilivyo maanake ni wa maana sana haswa kwa mazao ya maziwa. Maziwa yao yana ladha nzuri mno hata kuliko ya ng’ombe,’’ alisema Nyagarama.

Wakati uo huo, gavana huyo alisema kuwa serikali yake iliamua kuwapa makundi mbuzi hao huku akisema wakati uchao kila mtu atapokezwa mbuzi wakionekana kuwa waufugaji bora.

Aidha Gavana Nyagarama alisema kuwa mbuzi hao watawekewa mbegu ya Artificial Insermination ili mbuzi hao wapate wanao wenye afya bora na kuongezeka ndio watu wawe na maendeleo ya kibiashara.

“Kuna maafisa wa ufugaji ambao watatembea kwa makundi kuthibitisha kuwa mbuzi hao wanahitaji kupata mbegu ya kuzalisha ili wapewe mara moja,’’ alidokeza Gavana Nyagarama.

Kwa upande mwingine wakaazi wa Kaunti hiyo walionekana kuwa na furaha kwa kile gavana wao ameanzisha huku wengi wakisema kuwa wana imani kuwa Kaunti yao itainuka kiuchumi.

“Tunamshukuru Gavana Nyagarama kwa mradi wa mbuzi. Sasa tuna imani kuwa Kaunti yetu itaendelea mbele na tunamuomba kila gavana wetu awape watu wote mbuzi iwapo kama ataendelea na mradi huo wala si kwa makundi tu,’’ alihoji Andrew Magara mkaazi Nyamira