Gavana wa kaunti ya Nyamira John Nyagarama amewahimiza wanasiasa wanaowania nyadhifa mbalimbali za kisiasa kukumbatia amani na heshima miongoni mwao.
Akihutubu kwenye hafla ya kuchangisha pesa za ujenzi wa parukia ya kanisa katholiki kule Riomego siku ya Jumapili, Nyagarama alisema sharti wanasiasa waheshimiane ili kuepusha uwezekano wa kuzuka vita miongoni mwa wafuasi wa wagombezi vyeo mbalimbali.
"Uwaniaji nyadhifa za kisiasa sio uadui, na ndio maana nawahimiza wanasiasa wanaowania nyadhifa mbalimbali za kisiasa kuheshimiana ili kuepuka uwezekano wa kuzuka vurugu miongoni mwa wafuasi wao," alisema Nyagarama.
Nyagarama aidha aliwahimiza wakristu kuliombea taifa tunapoelekea kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2017.
"Utangamano ni muhimu sana kwa ukuaji wa taifa hili na ni ombi langu kwa wakristu kuliombea taifa hili tunapoelekea kwenye uchaguzi mkuu ujao," aliongezea Nyagarama.