Mbunge wa eneo la Mugirango magharibi Dkt James Gesami amepata uungwaji mkono kuchukua uongozi wa chama cha ODM tawi la Nyamira baada ya mwenyekiti wa sasa ambaye pia ni mbunge wa Kitutu Masaba kutangaza kuwa nia yake ni kuzingatia majukumu ya kitaifa ya chama hicho hasa ya uweka hazina.
Akizungumza katika eneo la Kebirigo alipopata uungwaji mkono wa kiongozi wa walio wengi kwenye bunge la kaunti ya Nyamira Laban Masira na mwakilishi mwenzake wa wadi ya Bogichora Beautah Omanga, Gesami alisema kuwa ana imani ya kuibuka na ushindi kwenye uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi Novemba.
"Mimi ni mwanachama mwaminifu wa chama cha ODM, na kwa siku nyingi nimekuwa nikisimama na chama hata kwenye wakati mgumu, na kwa sababu hiyo nina hakika kuwa nitachaguliwa kuongoza chama hicho huku nyamira ili kusaidia kukiimarisha hata zaidi," alisema Gesami.
Kiongozi wa walio wengi kwenye bunge la kaunti ya Nyamira Laban Masira alisema kuwa wanachama wa ODM kwenye bunge la kaunti ya Nyamira wana hakika kuwa Gesami atadhihirisha uongozi mzuri ikizingatiwa kwamba ana tajriba ya miaka mingi kwenye uongozi.
"Ningependa kuwambia wafuasi wetu kuwa sisi kama wawakilishi wa wadi wa mlengo wa ODM tuna hakika kuwa mheshimiwa Gesani atatuongoza vizuri," alisema Masira.
Akimshukru mwenyekiti anayeondoka wa chama hicho, mwakilishi wa wadi ya Bogichora Beautah Omanga alisema kuwa uongozi wa mbunge Timothy Bosire ulikuwa wa kutiliwa mfano, huku akiongeza kuwa sasa wako tayari kwa uongozi wake Gesami.
"Ningependa kumshukru Bosire kwa uongozi wake mzuri na tunatarajia kuwa atatuwakilisha vizuri kwenye afisi ya hazina ya kitaifa ya chama kwa kuwa sasa tuko tayari kwa uongozi wake Gesami," alisema Omang'a.
Haya yanajiri baada ya mbunge wa Kitutu Masaba kutangaza kule Gekano kuwa hakuwa na nia ya kuwania cheo hicho kwa mara nyingine, hali iliyotoa fursa kwa mbunge wa Africa mashariki Joseph Kiangoi na yule wa Mugirango magharibi kungangania cheo cha uenyekiti wa chama Nyamira.