Kuafutia hatua ya baadhi ya mawaziri wa serikali ya kitaifa kujitokeza kwenye mikutano ya hadhara na kuzungumzia masuala ya kisiasa kinyume ilivyo kikatiba, sasa mbunge wa Mugirango magharibi James Gesami amejitokeza kushtumu hali hiyo.
Akizungumza kwenye hafla ya mazishi kule Egesieri siku ya Jumapili, Gesami alisema kuwa ni hatia kwa maafisa wa umma kujihusisha na masuala ya kisiasa.
"Inakuwaje kwamba maafisa wa umma wanaweza kujihusisha na siasa ilhali kulingana na katiba kamwe hawaruhusiwi kujihuzisha na masuala yeyote ya aina hiyo na ndio maana naona kama hiyo ni hatia kubwa," alisema Gesami.
Gesami aidha aliitaka tume ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC kuchunguza visa vya baadhi ya maafisa wa umma wanaojihusisha na siasa ili kuwachukulia hatua kali za kisheria.
"Nasihi tume ya IEBC ichukue jukumu la kuchunguza maafisa walio na tabia kama hizo ili wachukuliwe hatua za kisheria kwa maana ni kinyume cha sheria na inawezekana kwamba maafisa wa aina hiyo wanatumia vibaya raslimali za umma kwa kujihusisha na siasa," aliongezea Gesami.
Haya yanajiri baada ya mawaziri wawili akiwemo waziri wa kawi Charles Keter na mwenzake wa maji Eugene Wamalwa kujihusisha hadharani kwenye kampeni za kisiasa.