Mwanamume mmoja anapigania maisha yake katika hospitali kuu ya wilaya ya Naivasha kufuatia ghasia mpya ambazo zimezuka eneo la Kosovo mjini Naivasha siku ya Jumatatu.
Hatua hiyo imeifanya kamati ya usalama ya wilaya hiyo kuzuru eneo hilo ambalo limekuwa likikumbwa na ghasia za kila mara huku zaidi ya watu watano wakiaga dunia.
Mkaazi mmoja, Simon Kimei alisema; “Mwanamume huyo alikuwa akielekea shambani mapema leo (Jumatatu) wakati alivamiwa na kikundi kimoja cha vijana kutoka jamii moja inayozozania umiliki wa ardhi na jamii nyingine.”
Naibu wa mkuu wa kaunti ndogo ya Naivasha John Opondo alisema kuwa mhasiriwa huyo alidungwa mikuki mitatu mwilini mwake na kukimbizwa hospitalini akiwa katika hali mahututi.
Akizungumza kwa njia ya simu na mwanahabari huyu, Opondo aidha aliongeza kuwa maafisa zaidi wa usalama wametumwa eneo hilo ili kuweza kurejesha hali ya usalama.