Mwakilishi wa wadi ya Nyota katika bunge la ngatuzi la Nakuru, Njuguna Gichamu, ameitaka Serikali Kuu kuongeza idadi ya waalimu katika eneo hilo.
Gichamu amesema kuwa tangu serikali ianzishe mpango wa elimu bila malipo idadi ya wanafunzi wanaojiunga na shule za umma imeendelea kuongezeka.
Amesema licha ya mpango huo kulenga wanafunzi kutoka jamii maskini, serikali haijaweka sera madhubuti ya elimu ili kukabiliana na changamoto ibuka.
“Shule za msingi na upili katika maeneo ya mashambani zimesahaulika kabisa.Wazazi hapa wanalazimika kulipa malipo zaidi ili kuajiri waalimu zaidi. Shule zingine zenye zaidi ya wanafunzi 700 zina walimu 6 pekee wa kuajiriwa na serikali,” akasema Gichamu.
Kiongozi huyo amesema serikali imekuwa ikijikokotakokota badala ya kujaza nafasi za walimu waliostaafu, kufutwa kazi ama kufariki.
Akiongea katika shule ya upili ya Karirikania, Gichamu alisema kuwa upungufu wa walimu unaathiri elimu na ni sharti waziri wa elimu Jacob Kaimenyi atatue tatizo hilo.
“Uhaba wa waalimu ndio chanzo cha matokeo duni katika mitihani ya kitaifa. Sioni kama ni haki kuwapa wanafunzi wa shule hizi za mashambani mtihani mmoja na wale wanafunzi walioko katika shule za hadhi za juu,” akaongeza Gichamu.
MCA huyo amesema baadhi ya walimu hupewa uhamisho kwa vigezo kwamba mashambani kuna mazingira magumu ya kufanyia kazi akipendeka serikali kuajiri walimu wanaofahamu vyema maeneo wanayotumwa kutoa huduma zao.
Gichamu ametamatisha kwa kusema baada ya machafuko ya mwaka 2007-2008 kubwa ya walimu waligura wilaya Kuresoi na hadi sasa serikali haijajaza pengo zilizoachwa.