Mbunge wa Nakuru mjini mashariki David Gikaria amepinga vikali madai kwamba hajatekeleza miradi maalumu ya maendeleo katika eneo bunge lake.
Akizungumza mjini Nakuru, Gikaria alipuuzilia mbali swala hilo na kutaja habari hizo kama uvumi tu na juhudi za wapinzani wake kumharibia sifa.
Alisema kuwa katika eneo bunge lake ana hakika ameshatekeleza miradi maalumu ya maendeleo, na kuongeza kuwa alishatekeleza miradi aslimia 60 katika kipindi kifupi.
Wakati huo huo, alitaka vyombo vya habari kumakinika na kuripoti kuhusu miradi ya maendeleo.
"Nyinyi pia wanahabari, msiwe tu wa kutangaza wakati mbunge amehusika na ufisadi, bali pia mjaribu kuandika kuhusu miradi ya maendeleo," alisema Gikaria.
Alisisitiza kwamba atawania tena kiti cha eneo bunge la Nakuru mjini Mashariki mwaka 2017.