Mbunge wa Nakuru Mashariki David Gikaria amewahimiza wakaaji wa mji wa Nakuru kuimarish utulivu na amani licha ya mambo mengi yanayoendelea katika mji huo ambayo yanaweza kuhatarisha amani.
Gikaria alisema haya jana nje ya mahakama ya Nakuru, baada ya kuhudhuria kusikilizwa kwa kesi iliyowasilishwa mahakamani na Kundi la wachuuzi mjini Nakuru kuipinga serikali ya jimbo kuhamisha wachuuzi kutoka katikati ya mji wa Nakuru, huku vibanda vyao vikibomolewa.
Gikaria aliwataka wachuuzi na wakaaji wengine wa Nakuru kuwa wavumilivu, huku wakingoja maamuzi ya mahakama, akishikilia kuwa haki lazima itendeke.
Alikosoa serikali ya jimbo ikiongozwa na Gavana Kinuthia Mbugua kwa kutojali masilahi ya wachuuzi zaidi ya elfu thelathini mjini Nakuru, ambao ni maskini wanaojaribu kujitafutia riziki.
“Sielewi ni kwa nini serikali ya jimbo inatoa amri kama hizi bila kujadili hali ya umasikini inayokumba watu kama hawa wachuuzi. Hawa wananchi wanajaribu kujitafutia riziki na serikali inafaa iwainue badala ya kuwarudisha chini zaidi,” alisema Gikaria.
Aliongeza kuwa yeye kama kiongozi, hatachoka kamwe kutetea haki za waliomteua, na atahakikisha ya kwamba haki imetendeka.
Gikaria aidha aliwakashifu polisi kwa kutumia nguvu katika kazi zao, na kutishia kuwachukulia hatua ya kisheria afisa wa polisi ambao Jumapili iliyopita walimvamia na kumudhuru kimwili, alipokua akiwaongoza wachuuzi katika maandamano ya kupinga kuhamishwa kutoka kati ya mji