Mbunge wa Nakuru mjini mashariki David Gikaria ametoa wito kwa akina mama na vijana waliosajiliwa katika mradi wa vijana kupitia shirika la huduma kwa vijana NYS kutumia fursa hiyo kujiimarisha.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Akizungumza siku ya Jumatatu katika eneo la Free Area baada ya kufanya mkutano na vikundi mbalimbali vilivyosajiliwa katika mradi huo, Gikaria alisema kuwa mradi huo kwa sasa utaendelea pasina pingamizi lolote baada ya kukumbwa na utata katika siku za awali.

Alisema kuwa mradi huo ni mojawapo ya mbinu ya serikali ya Jubilee kuhakikisha kwamba inawapiga jeki vijana na akina mama kwa kuhakikisha wanajiimarisha na kuinua uchumi wa taifa.

"Ningependa kuwafahamisha kwamba mradi huu sasa umeng'oa nanga. Nawaomba wale wote waliosajiliwa kuhakikisha kwamba wanatumia fursa hii vyema katika kujinufaisha," alisema Gikaria.

Wakati huo huo, mbunge huyo aliwataka wale waliotuma maombi ya kupata fedha za hazina ya Uwezo katika eneo bunge lake kuwa watulivu., kwani fomu za maombi zinapigwa msasa katika afisi kuu jijini Nairobi.

Aidha, alipuuzilia mbali madai ya baadhi ya makundi ya vijana kwamba fedha hizo zinatolewa kwa njia ya mapendeleo.

Alisisitiza kuwa wale wote waliohitimu watapata fedha hizo kwa njia ifaayo.