Mkuu wa sheria Dkt Githu Muigai amepewa siku saba kueleza njia iliyotumika kuteua makamishna wapya wa Waqfu wa Kiislamu nchini.

Share news tips with us here at Hivisasa

Hii ni baada ya makamishna Sheikh Juma Ngao, Shariff Hussein Ahmed, Prof Hamadi Boga, Noor Zubeir Hussein, Nagib Shamsan, na Dkt Mwanakitini Bakari kuteuliwa kusimamia mali ya jamii ya Kiislamu.

Wakili Luta Nduta, kutoka afisi ya mkuu wa sheria alikuwa ameomba muda wa siku 14 kuweza kuweka wazi ripoti kuhusu uteuzi huo.

Hatua hiyo ilipingwa na wakili wa makamishna hao, Yusuf Aboubakari, aliyesema kuwa afisi ya mkuu wa sheria ipewe siku saba pekee.

Jaji Mathew Emukule, anayesikiza kesi hiyo ameipa afisi ya mkuu wa sheria siku saba, kuweka wazi namna uteuzi wa makamishana hao wapya ulivyotekelezwa.

Ikumbukwe kuwa aliyekuwa Kadhi Mkuu wa Kenya Sheikh Hammad Kassim na wengine waliishtaki afisi ya Mkuu wa sheria Githu Muigai kuhusu uteuzi wa makamishna hao.

Kesi hiyo itasikizwa tena Oktoba 12, mwaka huu.