Aliyekuwa mbunge wa zamani wa eneo bunge la Mugirango kaskazini Godfrey Masanya ameaga dunia baada ya kuugua kwa muda mfupi.
Akithibitisha kisa hicho, mpwa wa mwendazake Jones Omweng'a anayehudumu kwenye wadhifa wa waziri wa elimu katika kaunti ya Nyamira alisema Masanya aliyefariki kwenye hospitali ya kibinafsi St. Leornad kule Kericho jumapili jioni, na amekuwa akiugua maradhi ya kisukari kwa muda sasa.
“Mheshimiwa mwendazake aliaga Jumapili jioni baada yake kupelekwa kwenye hospitali ya St. Leornald kule Kericho na huenda ugonjwa wa sukari ukawa chanzo cha kifo chake,” alisema Omweng'a.
Kwa upande wake mbunge eneo wa eneo bunge la Borabu Ben Momanyi, aliyekuwa miongoni mwa viongozi waliofika kwenye hospitali hiyo baada ya kupokea ripoti ya kuaga kwa mwendazake, ametuma risala za rambirambi kwa jamaa na wakazi wa eneo bunge la Mugirango kaskazini.
“Kwa kweli tumempoteza kiongozi mkomavu na shupavu sana ambaye wakati wa uhai wake alijaribu sana kupigania haki za wapiga kura wake, na kwangu mimi ninawapa risala za rambirambi wote waliompenda Masanya,” alisema Momanyi.
Ikumbukwe kuwa Masanya aliwahi kuhudumu kwenye wadhifa wa ubunge kwenye eneo bunge la Mugirango kaskazini kati ya mwaka wa 2002-2007.