Shirika la kutetea haki za binadamu la Haki Africa limewashutumu maafisa wa polisi kwa kutumia nguvu kupita kiasi wakati wa maandamano dhidi ya Tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Akiwahutubia wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumanne, mkurugenzi mkuu wa shirika hilo Hussein Khalid alitoa wito kwa serikali kuwatia mbaroni maafisa wa polisi waliowadhulumu waandamanaji.

Khalid alisema kuwa ni kazi ya polisi kulinda usalama wa wananchi na mali yao, wala sio kuwakandamiza na kuwaumiza kwa kutumia nguvu zisizo na kipimo.

“Ni jambo la kusikitisha kuona polisi wakiwakandamiza wananchi na kukiuka haki za kibinadamu. Tabia hiyo sharti ikomeshwe mara moja,” alisema Khalid.

Haya yanajiri baada ya kanda na picha tofauti kusambazwa katika mitandao ya kijamii ikionesha jinsi polisi walivyowapiga wafuasi wa mrengo wa Cord wakati wa maandamano ya kushinikiza kubanduliwa kwa Tume ya IEBC siku ya Jumatatu.