Shirika la kutetea haki za binadamu la Haki Africa linataka kujumuishwa kwa mazungumzo kuhusiana na Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC.
Akizungumza siku ya Jumamosi, Mkurugenzi mkuu wa shirika hilo Hussein Khallid, alisema maswala ya uchaguzi sio ya kisiasa pekee bali yanajumuisha mashirika ya kijamii yanayohusiana na haki za binadamu.
“Tunaomba kujumuishwa pamoja na mashirika mengine ya kijamii ili kuzuia ukandamizaji wowote wa mwananchi kwa njia moja ama nyengine,” alisema Khallid.
Aidha, Khallid alisema kuwa mgogoro huo unajumuisha maswala ya kikatiba na haki za mwananchi kuchagua kiongozi wake, hivyo basi haitakua jambo la busara kuwachia mazungumzo hayo wanasiasa na Tume hiyo ya IEBC pekee.