Shirika la kutetea haki za binadamu la Haki Afrika limezindua mradi wa kuhamasisha wananchi kuhusu haki zao ili kukabiliana na ongezeko la visa vya uhalifu Mombasa.

Share news tips with us here at Hivisasa

Shirika hilo lililo na makaazi yake jijini Mombasa, limesema kuwa mradi huo utafanikisha pakubwa utendakazi wa pamoja kati ya wananchi, mashirika ya kijamii na idara ya polisi.

Mkurugenzi mkuu wa shirika hilo Hussein Khalid amesema kuwa mradi huo unanuia kuboresha usalama.

Khalid alisema kuwa ana imani kuwa kuboreshwa kwa usalama Mombasa kutatoa mazingira ya kuboresha sekta ya utalii.

“Tunataka kuwa na sura mpya katika maswala ya uhusiano kati ya idara ya usalama, mashirika ya kijamii na wananchi. Sisi kama shirika tunanuia kutekeleza kazi hiyo kuhakikisha kuwa wananchi na idara ya usalama wanafanya kazi kwa kushirikiana bila uhasama,” alisema Khalid.

Aidha, mkurugenzi huyo alionesha kugadhabishwa kwake na tabia ya kulaumiana na kunyosheana vidole pindi mkasa unapotokea, badala ya kutafuta suhulu.

Wakaazi katika jiji la Mombasa wamekuwa wakiilaumu idara ya polisi kwa kile walichokitaja kama kunyanyaswa kwa haki zao za kibanadamu, hali ambayo imepelekea ushirikiano katika ya idara ya polisi na wanachi kudorora.