Shirika la kutetea haki za binadamu la Haki Afrika limeandaa mswada unaolenga kuwalinda Wakenya wanaofanya kazi za yaya, katika mataifa ya kigeni hasa Uarabuni dhidi ya mateso mikononi mwa waajiri wao.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza na mwandishi huyu afisini mwake siku ya Jumanne, afisa mratibu wa mipango katika shirika hilo, Francis Gamba, alisema kuwa wanalenga kuwasilisha mswada huo bungeni katika siku za hivi karibuni ili upitishwe kuwa sheria.

Gamba alisema kuwa wameafikia hatua hiyo ili kulinda na kutetea haki za Wakenya ambao mara nyingi hudhulumiwa na waajiri wao hasa wanaofanya kazi katika mataifa ya Milki za Kiarabu.

“Tumechoka kupokea miili ya Wakenya ambao huteswa na kisha kufarika kinyama Ughaibuni. Wakati umefika mawakala na maajenti wanaowasafirisha katika mataifa hayo wachukuliwe hatua za kisheria,” alisema Gamba.

Afisa huyo aidha alidokeza kuwa baadhi ya vipengele katika mswada huo vinahitaji kuwa kabla ya kusafirishwa kuwa mfanyikazi wa nyumbani Ughaibuni, sharti serikali ijulishwe kwa mwajiri anayepania kumuajiri Mkenya huyo.

Kwa mujibu wa takwimi za Haki Afrika, zaidi ya visa 16 vya Wakenya kudhulumiwa na waajiri wao katika mataifa ya nje tayari vimeripotiwa kati ya mwezi Januari na Aprili mwaka huu.