Shirika la kutetea Haki za binadamu la Haki Afrika limehimiza jamii kutowatenga vijana wanaorandaranda mitaani na badala yake watangamane nao ili kuwasaidia kuyarejelea maisha yao ya kawaidi.
Akizungumza na mwandishi huyu afisini mwake siku ya Jumatano, afisa msimamizi katika shirika hilo, Salma Hemed, alisema kuwa tayari wamelianzisha zoezi la kutoa hamasa kwa wazazi, walimu na wadau wengine mjini humo kuhusiana na namna ya kuwasaidia vijana hao kujikimu kimaisha.
Afisa huyo alifichua kuwa wamechukua hatua hiyo ili kupunguza visa vya vijana wanaorandaranda mitaani kusajiliwa na makundi haramu kama al-Shaabab, hasa baada ya takwimu zilizotolewa na shiriki la kutetea haki za binadamu la Huria mapema mwezi huu kuonyesha kuwa idadi hiyo inazidi kuongezeka.
“Kama shirika tunahofia usalama wa vijana hawa kutokana na namna wanavyochukuliwa na jamii, maisha yao ya kila siku na hatari wanayojiweka wapaojiunga na makundi haramu,” alisema Hemed.
Aidha, mtetezi huyo wa haki za kibinadamu alisema kuwa Haki Afrika tayari imekuja na mpango wa kuwahusisha vijana hao katika michezo mbalimbali kama njia moja ya kuwaleta karibu na jamii.
Kwa muda sasa vijana wanaorandaranda mitaani katika eneo la Pwani hasa mjini Mombasa wameripotiwa kusajiliwa na makundi yaliyoharamishwa, hatua ambayo imetajwa na Idara ya Usalama mjini humo kama hatari kwa usalama wa nchi.