Shirika la kutetea haki za binadamu la Haki Afrika limeshtumu vikali kukithiri kwa visa vya mauaji ya maafisa tawala katika eneo la Pwani.Mkurugenzi mkuu wa Shirika hilo, Hussein Khalid, amesema kuwa maafisa wa utawala, manaibu wao, wazee wa mtaa na wale wa nyumba kumi wanafaa kupewa ulinzi dhabiti kwani husaidia katika maswala muhimu nchini.

Share news tips with us here at Hivisasa

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari siku ya Jumatatu, Khalid alisema kuwa ni jambo la kusikitisha kuona watu wanaochangia kudumishwa kwa amani na usalama wakiuawa katika hali ya kutatanisha.

"Kama shirika, tunataka kuona maafisa tawala na manaibu wao, wazee wa mtaa na wale wa nyumba kumi wakipewa ulinzi kwani wanachangia kuimarishwa kwa usalama nchini. Serikali ni lazima iwaangazie,” alisema Khalid. 

Khalid aidha ameitaka idara ya usalama eneo la Pwani kuchunguza wanaohusika na mauaji hayo ili watiwe nguvuni.

Alisema kuwa swala hilo linafaa kutatuliwa haraka kwani hali hiyo huenda ikawatia hofu wakaazi wengi hasa wale wanaoishi mashinani.

Kauli ya mwanaharakati huyo inajiri baada ya afisa tawala katika Kaunti ya Lamu kuuawa na watu wasiojulikana alipokuwa akielekea kazini siku ya Ijumaa.