Mashirika ya kutetea haki za binadamu yamemkosoa Rais Uhuru Kenyatta kwa kutia saini mswada wa marekebisho ya sheria za uchaguzi.
Kwenye kikao na wanahabari mjini Mombasa, afisa kutoka shirika la Haki Africa Francis Auma alisema kuwa uamuzi aliochukua Rais Kenyatta ulifanywa kwa haraka na huenda ukazua taharuki miongoni mwa Wakenya.
Auma alisema kuwa ingekuwa vyema iwapo rais angewahusisha wananchi katika uamuzi huo, ili kuhakikisha kuwa kuna amani nchini.
Wakati huo huo, amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kwenye zoezi la kuwasajili wapiga kura, kwa kusema kuwa hiyo ndio njia ya pekee ya kuwawezesha kuwachagua viongozi bora.
Auma aidha alikosoa hatua ya Gavana wa Mombasa Hassan Joho na mwenzake wa Kilifi Amason Kingi kupokonywa walinzi wao.
Alisema kuwa hatua hiyo ilitekelezwa kaitika misingi ya dhulma na unyanyasaji, kwani magavana hao wanahaki kikatiba kuwa na walinzi.
Alisema ni jambo la kusikitisha kuona jinsi viongozi wa kisiasa wanavyoendeleza siasa zao katika hali ya chuki, hatua aiyosema huenda ikasababisha mgawanyiko miongoni mwa wananchi.
Auma aidha amewataka viongozi wa kisisa kujishugulisha na maswala ya kuleta maendeleo bila kujali siasa za vyama ili kukuza uchumi wa nchi.