Shirika la kutetea haki za kibinadamu nchini Haki Afrika limeshinikiza kubanduliwa kwa Tume ya Uchaguzi na uratibu wa mipaka nchini IEBC, ikidai kuwa kuendelea kusalia kwa Makamishna wa tume hiyo madarakani huenda kukachangia machafuko wakati wa uchaguzi mkuu ujao.
Afisa wa Haki na Sheria katika Shirika hilo, Francis Auma Gamba amesema kuwa idadi kubwa ya Wakenya hawana imani tena na tume hiyo na huenda ikachangia ukosefu wa usalama humu nchini kutokana na kila Mkenya kushinikiza kwa maafisa wakuu wa tume hiyo kung’atuka.
Amesema kuwa mvutano wa mrengo wa upinzani Cord kushinikiza kubanduliwa kwa tume hiyo basi kunatia hofu Wakenya ya kuzuka kwa machafuko na kupendekeza maafisa hao kutafuata agizo la Wakenya ili uchaguzi mkuu ujao kufanyika kwa amani na haki.
"Tunawaambia makamishna wa IEBC kujiondoa kwenye tume hiyo ili kuzuia kushughudiwa kwa machafuko nchini wakati wa uchaguzi kwa sababu sioni maana ya wao kusalia kwenye tume hiyo na Wakenya hawana imani nao heri tu waondoke kwa amani ili kenya iwe huru," alisema Auma siku ya Alhamis mjini Mombasa.
Wakati uo huo amewataka Wakenya kuzidi kudumisha amani na kutokubali kushawishiwa vibaya na baadhi ya viongozi wa kisiasa kwani kuzua mgogoro sio suluhisho la kutatua jambo huku akisema kuwa tayari wameanzisha hamasisho kwa vijana na jamii kwa julma kudumisha amani.
Kauli ya mwanaharakati huyo wa kijamii imejiri huku viongozi wa upinzani, wale wa kidini na wadau mbalimbali kushinikiza Maafisa wakuu wa Tume ya IEBC kung’atuka madarakani.