Hisia mseto zingali zinaibuka kuhusu hatua ya bunge la kitaifa kukosa kuupitisha mswada wa usawa wa jinsia.

Share news tips with us here at Hivisasa

Wanaharakati wa haki za binadamu wakiwemo wale wa Shirika la Haki Afrika, sasa wanashinikiza bunge hilo livunjiliwe mbali kwa kushindwa kuitekeleza katiba kikamilifu.

Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo Hussein Khalid, alisema kuwa ni jambo la kusikitisha kuwaona wabunge wakiupinga mswada huo ulioandaliwa kwa kuzingatia katiba ya sasa.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Ijumaa, Khalid alisema shirika hilo litashirikiana na wanaharakati wa mashirika mengine kuwahamasisha wabunge kuhusu umuhimu wa suala la uwakilishi wa jinsia uongozini.

“Tutafanya kila juhudi kushirikiana na mashirika mengine kuwahamisisha wabunge kuhusu umuhimu wa maswala ya uwakilishi wa jinsia ya uongozi hasa mswada huu wa thuluthi mbili,” alisema Khalid.

Itakumbukwa kuwa siku ya Alhamis wabunge walikosa kuupitisha mswada huo wa usawa wa jinsia ambao wengi wanasema utazidisha gharama za serikali iwapo utaidhinishwa.