Shirika la kutetea haki za binadamu la Haki Afrika limeitaka bunge kuvunjilia mbali Idara ya polisi nchini na kuliachia jeshi kuendeleza shughuli za usalama.
Hii ni baada ya idara hiyo kudaiwa kuhusika katika visa vya unyanyasaji na ukiukaji wa haki za binadamu na katiba ya taifa.
Kwenye mahojiano na mwanahabari huyu, afisa kutoka shirika la Haki Afrika Francis Gamba, alisema kuwa idara ya polisi imekuwa ikijihusisha na uvunjanji wa haki za binadamu nchini.
"Visa vingi vya unyanyasaji vinasababishwa na polisi nchini. Hatua za haraka zinapaswa kuchukuliwa dhidi ya polisi wanaovunja sheria,” alisema Gamba.
Akizungumza siku ya Jumamosi, Gamba alilalamika kuwa idara ya polisi haiko tayari kufanyiwa marekebisho ilhali inajihusisha na uvunjaji wa katiba.
Aliongeza kuwa itakuwa vyema iwapo polisi wapya wataajiriwa badala ya kufanya kazi na maafisa wanaowanyanyasa wananchi.
Aidha, ametaka kuchukuliwa hatua za kisheria kwa afisa wa polisi aliyehusika katika unyanyasaji wa afisa wa IPOA.
Kauli hii inajiri baada ya chama cha mawakili na IPOA kulaani vikali unyanyasaji dhidi ya maafisa wake.