Shirika la kutetea haki za binadamu la Haki Afrika linataka makamishna wa Tume ya uwiano na utangamano nchini NCIC kujiuzulu.

Share news tips with us here at Hivisasa

Kwenye mahojiano na mwandishi huyu afisini mwake siku ya Jumanne, Mkurugenzi wa Haki Afrika, Hussein Khalid, alisema hakuna haja ya makamishna hao kuzidi kusalia afisini huku wakijikokota kuwachukulia hatua watu wanatoa matamshi ya uchochezi.

Khalid alisema tume hiyo inayoongozwa na aliyekuwa Spika wa bunge la taifa Francis Ole Kaparo imeshindwa kutokomeza matamshi ya uchochezi yanayotolewa na viongozi nchini, na badala yake inashinda ikitoa vitisho visivyo na msingi wowote.

“Makamishna wa NCIC sharti wang’atuke. Taifa linahitaji watu wanaotekeleza wajibu wao kikatiba pasi na uwoga wowote,” alisema Khalid.

Afisa huyo wa kutetea haki za binadamu alielezea kukerwa kwake na namna NCIC inavyokosa kuwachukulia hatua kali wanasiasa wanaotoa matamshi yanayoweza kuzua mgawanyiko wa kikabili nchini, licha ya kesi nyingi zinazowahusu kuripotiwa.

“NCIC imedhihirisha kuwa haiwezi kuwaadhibu wanasia, hivyo makamishna hao wanapaswa waondoke watoe nafasi kwa wengine watakaowahudumia wananchi bila kujali cheo wala hadhi ya mtu,” aliongeza Khalid.

Haya yanajiri baada ya wabunge Moses Kuria wa Gatundu Kusini, Kimani Ngunjiri wa Bahati, Junet Mohammed wa Suna mashariki Timothy Bosire wa Kitutu Masaba na Seneta wa Machakos Johnson Muthama kufika mbele ya mkurugenzi wa CID kuandikisha taarifa kuhusiana na madai ya kutoa matamshi ya uchochezi.