Shirika la kutetea haki za binadamu la Haki Afrika linataka serikali kupiga marufuku matumizi ya miraa nchini kwa madai kuwa inachangia utovu wa nidhamu miongoni mwa wanafunzi.

Share news tips with us here at Hivisasa

Afisa wa mipango katika shirika hilo, Francis Auma, amesema kuwa kuhalalishwa kwa matumizi ya bidhaa hiyo kumefanya wanafunzi kuipata kwa urahisi na hivyo kuitumia vibaya na kisha kukosa maadili.

Kwenye mahojiano na mwandishi huyu afisini mwake siku ya Jumatatu, Auma alisema kuwa huenda matumizi ya mihadarati na dawa zingine za kulevya ndiyo chanzo cha uchomaji shule ambao umekuwa ukishuhudiwa katika shule nyingi nchini.

“Hatusemi miraa ni mbaya. Tunachotaka ni serikali kutafuta mbinu ya kudhibiti matumizi yake hasa miongoni mwa vijana shuleni,” alisema Auma.

“Ikiwa hilo halitawezekana, basi bidhaa hiyo ipigwe marufuku maana huenda miraa na dawa zingine za kulevya ambazo wanafunzi wanapata kwa urahisi ndiyo sababu kuu ya kushuhudiwa kwa migomo na uchomaji shule,’’ alisema Auma.

Auma aliongeza kuwa kama shirika la kutetea haki za binadamu, wameanzisha michezo mbalimbali ili kuwaleta vijana pamoja kama njia mojawapo wa kutoa hamasa kwao kuhusiana na athari za kutumia mihadarati.