Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Shirika la kutetea haki za binadamu la Haki Afrika linaitaka idara ya polisi kuwachukulia hatua baadhi ya watu wenye tabia ya kusambaza picha za washukiwa wa uhalifu kwenye mitandao ya kijamii.

Shirika hilo linadai kwamba kila mara washukiwa wanapokamatwa na kuna baadhi ya watu wanaowapiga picha na kuzisambaza kwenye mitandao na kuandika jumbe zinazoonyesha kwamba wao ni wahalifu hata kabla ya mahakama kutoa uamuzi wake.

Akizungumza na mwandishi siku ya Jumatatu afisini mwake, Francis Auma afisa wa Haki Afrika alisema kuwa tabia hiyo mi kinyume cha sheria na mahakama pekee ndio yenye mamlaka ya kuamua iwapo mtu ni mshukiwa au la.

“Watu wanapiga picha alafu wanaandika hapo chini kwamba hawa ndio wahalifu waliokamatwa ilhali kesi bado ziko mahakamani,” alisema Auma.

Afisa huyo alikuwa akitoa mfano wa tukio la wikendi iliyopita ambapo kundi la vijana lilikamatwa kwenye msako wa kuwasaka vijana wanaowahangaisha wakaazi usiku.

Zaidi ya vijana 15 walikamatwa, lakini baadae picha zao zikaanza kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii na baadhi ya watu.

Auma aliongeza kuwa wale walikuwa ni watoto wadogo chini ya miaka 18 na kulingana na sheria watoto kama hao hawafai kuwekwa adharani.

“Sheria hairuhusu watoto chini ya miaka 18 picha zao kuwekwa adharani, polisi wanafaa kuwafanyia uchunguzi na wakipatikana na makosa wataadhibiwa kulingana na kanuni za sheria,” aliongeza Auma.

Afisa huyo alisema kuwa hatua hiyo huwaathiri zaidi familia za washukiwa hao kila wanapoziona mitandaoni.

Aidha afisa huyo alisisitiza kwamba idara ya polisi na ile ya mahakama inafaa kuchunguza swala hilo na kukomesha tabia ya baadhi ya watu kusambaza picha za washukiwa kwenye mitandao.