Shirika la kutetea haki za binadamu la Haki Afrika limeanzisha mpango wa kuwaleta pamoja wanawake na kuwapa mafunzo maalum yatakayosaidia kuwakinga watoto wao dhidi ya kujiunga na makundi ya kigaidi.

Share news tips with us here at Hivisasa

Hatua hiyo ni njia mojawapo ya kukabiliana na ongezeko la vijana wanaojiunga na makundi ya kigaidi nchini.

Afisa wa maswala ya jinsia na haki za watoto katika shirika hilo Salma Hemed, alisema kuwa wameanzisha mpango huo ili kuhakikisha kwamba vijana hawajiungi na makundi ya kigaidi bali wanatafuta mbinu za kujikimu kimaisha.

Akizungumza na wanahabari katika ofisi za shirika hilo jijini Mombasa, Hemed alisema kuwa mpango huo umezinduliwa katika ukanda wa Pwani ili kupiga vita itikadi kali miongoni mwa vijana.

“Kundi hili ni la kusaidia wanawake kuweza kujua dalili za vijana wao kuwa na misimamo mikali, ili kuwazuia dhidi ya kujiunga na makundi ya kigaidi. Wanawake wengi tayari wamefaidika na mpango huu,” alisema Hemed.

Kauli ya mtetezi huyu wa haki za kibinadam inajiri huku serikali ikiwataka vijana waliojiunga na makundi ya kigaidi kama lile la al-Shabaab kujisalimisha na badala yake kuhusika katika miradi ya serikali itakayo wasaidia kujiendeleza kimaisha.