Hakimu mmoja katika Mahakama ya Mombasa amejiondoa kwenye kesi ya meli iliyozamishwa baharini baada ya kupatikana na dawa za kulevya.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Meli hiyo, 'Baby Iris Yacht' ilinaswa mwaka jana ikiwa na kilo 7.6 za heroin zenye thamani ya shilingi milioni 22.

Hakimu Julius Nange’a ambaye alikuwa anasikiliza kesi hiyo amesema agizo la serikali la kuchoma meli hiyo lilikiuka kanuni za sheria, ikizingatiwa ilikuwa ni ushahidi kwenye kesi hiyo.

Nange’a ameagiza faili ya kesi hiyo kukabidhiwa hakimu mkuu katika Mahakama ya Mombasa, kwa mwelekeo zaidi wa kesi hiyo.

“Faili ya kesi hii itapelekwa kwa hakimu mkuu kwa mwelekeo zaidi kuhusu kuendelea kwa kesi hii,” alisema Nange’a.

Aidha, hakimu huyo alisema agizo lililotolewa na serikali kuhusu kuchomwa kwa meli hiyo sio la usawa na kuamua kujiondoa kwenye kesi hiyo.

“Agizo la kuchomwa kwa meli hiyo linakiuka sheria na kulemaza kuendelea kwa kesi hii,” alisema Nange’a.

Haya yanajiri baada ya mawakali wa upande wa utetezi kuitaka afisi ya mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma pamoja na mahakama kuelezea liliko meli hiyo ambayo ni moja wa ushahidi katika kesi hiyo inayowakabiliwa wanaume watano.

'Baby Iris Yacht' ilizamishwa baharini mnamo mwezi Agosti mwaka jana baada ya serikali kutoa agizo la kuchomwa kwa meli hiyo.

Waziri wa usalama wa ndani Joseph Nkaisery, mkuu wa majeshi jenerali Samson Mwathethe pamoja na kamanda mkuu wa jeshi la wanamaji Levi Mghalu walishuhudia kuzamishwa kwa meli hiyo baharini.

Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutoa agizo la kuchomwa kwa meli yoyote itakayopatikana na dawa za kulevya nchini.