Hakimu mmoja katika Mahakama ya Mombasa amejiondoa kwenye kesi ya ugaidi inayowakabili wasichana wanne.
Washtakiwa, Maryam Said Aboud, Ummulkheir Sadri Abdalla, Khadija Abubakar Abdulakadir na Halima Adan wanaodaiwa kuwa wafuasi wa kundi la kigaidi la al-Shabaab walitiwa mbaroni mwaka jana katika eneo la Elwak huko Mandera.
Hakimu katika mahakama ya Mombasa, Simon Rotich, alisema kuwa itakuwa vigumu kuendelea na kesi hiyo baada ya afisi ya mkrugenzi mkuu wa mashtaka ya umma kumtaka kujiondoa kwenye kesi hiyo kwa dhana kuwa angependelea upande mmoja.
Rotich alisema kuwa ombi la afisi ya mkuu wa mashtaka ya umma limemfanya kujiondoa shingo upande ili haki kupatikana kwa pande zote.
Hatua hii inajiri siku tatu tu baada ya maafisa wa kupambana na ugaidi ATPU pamoja na afisi ya mwendesha mashtaka ya umma kuwasilisha ombi la kumuondoa hakimu huyo.
Siku ya Jumanne, Hakimu Simon Rotich alisisitiza kuwa juhudi zake za kufanikisha kesi hiyo kusikilizwa kwa haraka ndio chanzo cha kutakiwa kujiondoa katika kesi hiyo.
Kesi hiyo itatajwa tena siku ya Jumatatu ili hakimu mwingine kupewa fursa ya kuisikiliza.