Afisi ya mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma imemtaka Hakimu Simon Rotich kujiondoa katika kesi dhidi ya wasichana wanne wanaodaiwa kuwa wafuasi wa kundi la kigaidi la al-Shabaab.
Washtakiwa hao, Maryam Said Aboud, Ummulkheir Sadri Abdalla, Khadija Abubakar Abdulakadi na Halima Adan walikamatwa tarehe 27 mwezi Machi, katika eneo la El Wak huko Mandera.
Wakili wa washukiwa hao, Mwadzogo Hamisi, ametaka upande wa mashtaka kuwasilisha ombi hilo rasmi katika mahakama na kuelezea sababu za kutaka Hakimu Rotich kutosikiza kesi hiyo.
Kwa upande wake, Hakimu Rotich alisema kuwa kuendesha kwake kwa kesi hiyo kwa haraka huenda kukawa sababu ya kumtaka kutoendelea kusikiza kesi hiyo.
Upande wa mashtaka unatarajiwa kuwasilisha ombi la kutaka Hakimu Rotich kutoendelea kusikiza kesi hiyo siku ya Alhamisi kabla ya kusikizwa na kuamuliwa Ijumaa.