Hakimu anayesikiza kesi ya washukiwa wanne wa ugaidi ametakiwa kujiondoa kwenye kesi hiyo.
Afisi ya mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma imemtaka Hakimu Henry Nyakweba kujiondoa baada ya kuwaachilia kwa dhamana wasichana wanne wanaokabiliwa na tuhuma za ugaidi.
Ummulkheir Abdullah, Mariam Said Aboud na Khadija Abubakar walikamatwa eneo la Elwak huku Halima Aden akikamatwa katika Kaunti ya Machakos kwa tuhuma za ugaidi mwaka 2015.
Mwendesha mashtaka kutoka afisi ya mkuu wa mashtaka ya umma tawi la Mombasa Jamii Yamina amewasilisha ombi la kumtaka Hakimu Nyakweba kutosikiza kesi hiyo kwa kudai kuwa alikiuka katiba kwa kuwapa washukiwa hao dhamana.
Jamii amesema kuwa Hakimu Nyakweba hakuzingatia uzito wa kesi hiyo kabla ya kutoa dhamana.
“Itakuwa bora kesi hiyo kuhamishwa na kupewa hakimu mwengine,” alisema Jamii.
Haya yanajiri baada ya Hakimu Nyakweba kuwaachilia wasichana hao kwa dhamana ya shilingi laki tano wiki iliyopita.
Wakili wa wasichana hao, Hamisi Mwadzogo, amepinga kauli hiyo, kwa kusema kuwa hiyo ni njama ya serikali kukiuka haki na uhuru wa wateja wake.
Amesisitiza kuwa yuko tayari kuelekea katika mahakama yoyote ambayo upande wa mashtaka inataka kesi hiyo kusikizwa.
Mwadzogo ameitaka mahakama kuu kutokubali ombi la upande wa mashtaka na kuiomba kutofutilia mbali dhamana iliyopewa wateja wake.
Si mara ya kwanza kwa upande wa mashtaka kutaka mahakimu wanaosikiliza kesi hiyo kujiondoa pindi wanapo waachilia washukiwa hao kwa dhamana.
Mwaka jana, Hakimu Simon Rotich alijiondoa kwenye kesi hiyo baada ya afisi ya mwendesha mashtaka kutokuwa na imani naye.
Mahakama itatoa uamuzi wake Februari 16.