Hakimu mkuu katika mahakama ya Mombasa Teressia Matheka ameomba muda zaidi ili kupitia faili ya kesi ya ugaidi inayowakabili wasichana wanne.

Share news tips with us here at Hivisasa

Hakimu Matheka amesema imemlazimu kuchukuwa muda huo ili kuipitia faili hiyo kabla ya kuikabidhi kwa hakimu mwengine ili aweze kuisikiliza.

Aidha, ameongeza kuwa atatumia muda huo ili kufanya ushahuri na hakimu Simon Rotich aliyekuwa akiisikiliza kesi hiyo kabla ya kujiondoa kwake.

Siku ya Jumanne, Matheka, aliahirisha kesi hiyo hadi siku ya Alhamisi, ambapo atatoa agizo la ni hakimu yupi atakayesikiliza kesi hiyo.

Haya yanajiri baada ya hakimu Simon Rotich kujiondoa kwenye kesi hiyo wiki iliyopita na kusababisha kulemaa kwa kesi hiyo.

Hii ni baada ya maafisa wa kupambana na ugaidi ATPU pamoja na afisi ya mwendesha mashtaka ya umma kuwasilisha ombi la kumuondoa hakimu huyo.

Siku ya Jumanne juma lililopita, hakimu Simon Rotich alisisitiza kuwa juhudi zake za kufanikisha kesi hiyo kusikilizwa kwa haraka ndio chanzo cha kutakiwa kujiondoa katika kesi hiyo.

Washtakiwa Maryam Said Aboud, Ummulkheir Sadri Abdalla, Khadija Abubakar Abdulakadir na Halima Adan wanadaiwa kuwa wafuasi wa kundi la kigaidi la Alshabab baada ya kutiwa mbaroni mwaka jana katika eneo la Elwak huko Mandera.