Kuna haja ya hamasa zaidi kutekelezwa mashinani kuhusu mbinu za kukabiliana na maambukizi ya virusi vya ukimwi ili kuzuia kuenea kwa virusi vya HIV katika eneo zima la Pwani.
Afisa mkuu wa Shirika linalopambana na ukimwi miongoni mwa akina mama nchini la ‘Women Fighting Aids in Kenya’, Ezekiel Kodonde amesema kuwa akina mama wengi wanaoishi na virusi vya ukimwi eneo la Pwani wanakabiliwa na changamoto.
Akizungumza katika afisi za shirika hilo eneo la Tudor mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Kodonde amesema kuwa ni sharti serikali za kaunti kushirikiana na mashirika yanayoangazia swala hilo la afya ili kuukabili unyanyapaa na kusaidia kupunguza maambukizi ya virusi vya ukimwi.
Kodonde amesema kuwa juhudi zinazotekelezwa na mashirika hayo nchini zinaashiria mafanikio makubwa katika kupigana na unyanyapaa na kuzuia kuenea kwa maambukizi ya virusi vya HIV.
“Tuko na matumaini kuwa lengo letu la kuangamiza ugonjwa huo litatimia kwa sababu changamoto kubwa na jamii kupata hamasa zaidi kuhusu maradhi hayo na kujikinga kutokana na maambukizi ya virusi vya HIV, basi tutajimudi zaidi na kuhakikisha kuwa janga hili tunakabiliana nalo,” alisema Kodonde.
Mwanaharakati huyo wa kupambana na maambukizi ya virusi hapa Pwani aliye pia afisa wa afya amezitaka serikali za kaunti kulipatia kipau mbele swala hilo la kukabiliana na maambukizi ya virusi vya ukimwi.