Gavana wa Mombasa Hassan Joho akiwahutubia mashabiki wa chama cha ODM katika uwanja wa Tonoka siku ya Jumapili. Picha: Hassan Joho/ facebook.com

Share news tips with us here at Hivisasa

Gavana wa Mombasa Hassan Joho amemkashifu Rais Uhuru Kenyatta kwa kile alichokitaja kama kumhangaisha.

Akizungumza muda mchache baada ya kuandikisha taarifa katika makao makuu ya polisi mjini Mombasa kwa tuhuma za kugushi cheti chake cha mtihani wa kidato cha nne KCSE, Gavana Joho alisema kuwa masaibu anayopitia kwa sasa hayatamsababisha kubadili msimamo wake wa kisiasa.

Vile vile, Joho alimkashifu Rais Kenyatta kwa kutumia nguvu nyingi kumhangaisha badala ya kuwatumikia Wakenya.

“Nina ushauri kwa Rais Uhuru Kenyatta. Hii nguvu na uwezo wa serikali unaotumia sasa kama kweli ungeutumia kwa niaba ya wananchi maisha ya Wakenya yangekua yamebadilika,” alisema Joho.

Gavana Joho alisema kuwa ni makosa kwa Rais Kenyatta kutumia nguvu za serikali kumhangaisha badala ya kukomesha ufisadi nchini na kupunguza gharama ya maisha kwa manufaa ya Wakenya.

Joho aidha alisema hamwogopi Rais Kenyatta licha ya kutishia kumnyorosha.

“Rais Kenyatta alikuja hapa Likoni na kutishia kuninyorosha na kuniangusha lakini mimi namwogopa Mungu pekee,” alisema Joho.

Joho vile vile aliwahakikishia wakaazi wa Mombasa kuwa atakua debeni mwezi Agosti, na kuongeza kuwa ana imani kuwa ataibuka mshindi.