Msimamizi wa usalama katika kaunti ya Kisii, Patrick Lumumba, amesema kuwa pesa wanabiashara wanazotozwa ushuru katika kaunti hiyo huwa zinawekwa kwenye benki kuu ya Kenya na si kwa benki ya kaunti hilo jinsi wengi hufikiria.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza jana na wanahabari katika mji wa Kisii, alisema wananchi wengi, wanabiashara wakiwa mojawao, hufikiria kuwa pesa hizo ambazo zinakusanywa  zinawekwa kwenye benki ya kaunti hilo, madai ambayo afisaa huyo aliyakana.

Aidha, Lumumba amewaomba wanabiashara kuendelea kutozwa ushuru wakitumia kiwango au bei ya zamani walizokuwa wakitoa hapo mbeleni, kama njia mojawapo ya kuzuia uchumi wa kaunti hiyo kurudi chini  na kudorora.

”wanabiashara wanafikiri kuwa pesa za ushuru katika kaunti hii yetu, huwekwa kwa akaunti ya serikali ya kaunti ya Kisii na kutumika vibaya. Nawahakikishia wananchi kuwa pesa zote za ushuru huwekwa kwa benki kuu ya Kenya na sio kwa benki ya kaunti yetu,”alisema Lumumba.

Wakati huo huo, msimamizi huyo wa usalama aliongezea kuwa kiwango cha pesa serikali ya kaunti hutoza kama ushuru, serikali ya kitaifa hukiangalia na kutumia kiwango hicho wakati serikali za kaunti zinapopokezwa pesa za maendeleo kutoka serikali ya kitaifa.

Alisema kua kama kaunti ilitoza  ushuru kwa kiwango cha chini, basi kiwango cha pesa kaunti husika hupokea hurudi chini vilevile.

“Pesa hizi zinakusanywa hapa kwa kaunti. Serikali ya kitaifa hufuatilia na kuthibitisha ni kiwango cha aina gani wakati kaunti zinapopokezwa pesa. Serikali kuu huwa inafuatilia halafu kaunti inapokezwa kulingana na jinsi kaunti ilitoza ushuru ,” alisema Lumumba.