Hata baada ya Rais Uhuru Kenyatta kusema kuwa serikali yake haiwezi mudu nyongeza ya mishahara kwa walimu, chama cha Kuppet tawi la Nyamira kimesisitiza kwamba wanachama wake hawatarejea darasani hadi pale serikali itakapowaongezea mishahara yao.
Akizungumza siku ya Jumatatu, katibu mkuu wa chama hicho, Lewis Nyakweba, alisema walimu hawapo tayari kurejea shuleni hadi pale matakwa yao yatakapotimizwa.
Nyakweba alisema yafaa serikali iheshimu maamuzi ya mahakama ya rufaa nakusisitiza kwamba wanachama wa Kuppet huenda wakarejelea maandamano ya barabarani kulalamikia hatua ya serikali kudinda kuwalipa nyongeza yao ya mishahara.
"Mahakama ya rufaa iliamuru tulipwe nyongeza ya kati ya asilimia 50-60 na yafaa serikali kuheshimu uamuzi huo na kwa kuwa hilo halijatimizwa, walimu wanachama wa muungano wa Kuppet wako tayari kurejea barabarani kwa maandamano makali zaidi,” alisema Nyakweba.
Akizungumzia swala la Rais Kenyatta kulinganisha mishahara ya walimu wa taifa hili na mataifa mengine ya afrika masharki na kati, Nyakweba alisuta ulinganishi huo akisema kwamba yafaa rais afahamu kuwa uchumi wa mataifa hayo hauwezi linganishwa na wa Kenya.
"Inashangaza kwamba Rais Kenyatta anaweza linganisha uchumi wa taifa hili na mataifa mengine ya afrika masharki, mataifa ambayo baadhi yao yanapambana kuimarisha uchumi wao,” alisema Nyakweba.
Mwenyekiti wa Kuppet tawi la Nyamira George Makau aliwaonya wanachama wa muungano huo watakaousaliti mgomo uliopo nakujihuzisha na usimamizi, ulinzi na usahihishaji wa mitihani ya kitaifa huku akiwasihi wazazi kutilia shaka mitihani hiyo iwapo itasimamiwa na vijana wa huduma ya NYS nchini.