Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka IEBC, imesema kuwa haitachukua maagizo ya jinsi ya kutekeleza jukumu lake kutoka kwa viongozi wa Cord.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Katika taarifa kwa vyombo vya habari siku ya Jumapili, IEBC ilisema kwamba inaweza tu kushirikisha umma pasi na kuwepo vitisho vyovyote.

Wakizungumza mjini Kitengela, Kaunti ya Kajiado, wakati wa sherehe za kufuzu kwa moran wa jamii ya Maasai, viongozi wa Cord Raila Odinga na Kalonzo Musyoka walisisitiza kuwa watafanya maandamano hadi afisi za IEBC siku ya Jumatatu, ili kuwaondoa makamishina wa tume hiyo ofisini.

Muungano huo wa Cord ulitishia kususia uchaguzi mkuu wa mwaka 2017 iwapo uchaguzi huo utasimamiwa na makamishna walioko mamlakani kwa sasa.

"Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka IEBC ni bodi huru kikatiba, iliyotwika jukumu la kusimamia chaguzi kuu na kura za maoni nchini Kenya. Tume hiyo haiwezi kuchukua maelekezo au maagizo kutoka kwa mtu yeyote au mamlaka yoyote katika utekelezaji wa majukumu yake,” ilisema IEBC katika taarifa.

"... IEBC inahitajika kushirikisha umma kwa ujumla na wadau maalum katika taratibu zake na maamuzi. Ushirikiano huo hata hivyo, unapaswa kufanyika bila ya vitisho vyovyote."

Tume hiyo ilisema imekuwa katika mawasiliano ya mara kwa mara na sekretarieti ya Okoa na muungano wa Cord kabla na baada ya uamuzi kuhusu kura ya maoni ya Okoa Kenya, iliyotupiliwa mbali.

IEBC ilisema inaitaka Cord na wananchi wote kudumisha utawala wa sheria kama inavyotarajia kutoka kwa wengine.

Tume hiyo ilisisitiza kuwa haitakubali kukabiliwa na shinikizo la jinsi ya kutekeleza majukumu yake, na kuongeza kuwa itahakikisha kuwa uchaguzi mkuu ujao utakuwa wa huru na haki.

"Tume hii itahakikisha kuwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2017 ni wa huru na haki. Hata hivyo, hayo hayawezi kuafikiwa iwapo tutakabiliwa na usumbufu wa maramara na misukosuko. Tunawaomba wananchi na wadau kutusaidia na kuwezesha juhudi za tume hii kuhakikisha uchaguzi huru na wa haki.”