Serikali ya Kenya imesema kuwa haitarudi nyuma katika kutekeleza uamuzi wake wa kuzifunga kambi za wakimbizi.
Akizungumza siku ya Ijumaa wakati wa mkutano na wajumbe wa Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, Rais Uhuru Kenyatta alisisitiza kuwa serikali itatekeleza mpango huo.
"Hatutarudi nyuma katika msimamo wetu wa kuzifunga kambi za wakimbizi kwa sababu usalama wetu ni muhimu sana,” alisema Rais Kenyatta.
Wajumbe hao waliitisha mkutano huo baada ya serikali kutishia kuzifunga kambi za Daadab na Kakuma ambazo zina zaidi ya wakimbizi laki tano kutoka nchi ya Somalia.
Serikali ya Kenya iliunda jopo la watu kumi na wanne lililotwikwa jukumu la kuchunguza mpango huo na tararibu mwafaka za kufanikisha kuzifunga kambi hizo.
Serikali imesema kuwa zoezi hilo la kuwarejesha wakimbizi kwao linafaa kuanza mwezi ujao.