Huku maandamano dhidi ya IEBC yanayoongozwa na mrengo wa upinzani Cord, yakishuhudiwa kila Jumatatu katika sehemu za Nairobi, Kisumu, Machakos na Kisii, wenzao kutoka mombasa wamepasua kimya chao kuhusu kutoshiriki maandamano hayo.
Wanachama wa Cord kaunti ya Mombasa hawakushiriki kamwe katika maandamano hayo.
Akiongea kuhusu sababu ya kutoandamana, Mwenyekiti wa ODM tawi la mombasa Bwana Mohamed Hatimy, alisema wanawangoja viongozi wao wa kaunti ndio wawaongoze katika maandamano.
"Hatuwezi fanya chochote sababu Bwana Joho hayuko mtaani na ndiye naibu kiongozi wa chama cha ODM," alisisitiza Bwana Hatimy.
Alisema wanamsubiri arudi nchini ndio atoe mwelekeo dhabiti."Tulikutana juma lililopita na viongozi wengine na kuonelea heri tumsubiri arejee ndio atupe njia," alisema hayo Bwana Hatimy.
Seneta wa Mombasa alidai yeye hana jibu lifaalo kulihusu swala hilo.
"Hatuna wasiwasi kabisa sisi na maandamano ya IEBC sababu sisi tunakuwa na amani sana kikazi na wanasiasa wa kaunti ya mombasa," alisema mkubwa wa eneo la mashariki na magharibi IEBC mombasa Bwana Abdulwahid.