Mwakilishi wa wadi ya Freretown ametoa matamshi kuhusiana na baadhi ya viongozi wa Pwani kutoa matamshi yanayoashiria uhasama baina yao kwa kukejeliana katika miradi mbalimbali.
Amir Thoya mwakilishi wa wadi ya Freretown, amewataka viongozi wa kisiasa kutoka Pwani kuwa waangalifu zaidi na namna wanavyoendesha siasa zao akisema huenda ikawaletea uhasama mkubwa miongoni mwao kwani kwa sasa kumekuwa na mgawanyiko mkubwa baina ya viongozi kuhusiana na muungano wa jumuia ya kaunti za Pwani akisema kuwa haipaswi kukejeliana hadharani kama kweli walikuwa wameafikiana kuungana kwa manufaa ya mkazi wa Pwani.
Akizungumza katika afisi yake iliyoko Freretown, Thoya amesema kuwa si vizuri kwa viongozi wa Pwani kuhubiri siasa zinazowatenganisha wakazi wa Pwani kwa kuwa sio siasa zilizowaweka kwenye nyadhifa bali ni sera zao walizotoa kwa wananchi na hivyo basi inapaswa kuzishuhulikia kabla ya muda wao wa kuondoka ofisini kukamilika mwaka ujao.
Thoya aidha amesema kuwa hatua ya baadhi ya viongozi wa Pwani kuhama mirengo waliyotumia kupata nyadhifa ni ishara tosha kwa viongozi hao kuwa kutakuwa na mgawanyiko mkubwa wa viongozi jambo ambalo anasema litawafanya wakazi wengi wa eneo la pwani kupoteza matumaini kwa viongozi wao kuanzia magavana hadi wawakilishi wa wadi.
Akitoa mfano wa hivi punde ambapo kumekuwa na mvutano wa iwapo fedha za jumuia ya kaunti za Pwani zinatumika namna gani, Amir amesema kuwa utumizi wa fedha za umma sio rahisi bali hadi kamati iliyochaguliwa kushuhulikia miradi iliyowekwa na baraza la jumuia ya pwani kuangazia namna watakavyoanza kutekeleza miradi hiyo.
Hata hivyo ameongeza kuwa ni sharti viongozi wote washirikiana ili mkazi wa Pwani apate kufaidika na miradi hiyo.